Corona: Watu 1,641 Wamekufa Nchini Brazil Kwa Siku Moja

 

Brazil imerekodi idadi kubwa ya vifo vinavyotokana na ugonjwa wa Covid-19 kwa siku baada ya watu 1,641 kufariki kwa ugonjwa huo. 

Wakati huo huo Rais wa Marekani Joe Biden ameahidi kuwepo kwa chanjo ya kutosha itakayomfikia kila mtu nchini humo kufikia mwisho wa mwezi Mei.

Kwa mujibu wa takwimu za wizara ya afya nchini Brazil, idadi hiyo ni kubwa ikilinganishwa na vifo 1,595 vilivyotokea kwa siku moja mwishoni mwa mwezi Julai, mwaka 2020.

Nchi hiyo ya America ya Kusini yenye idadi ya watu milioni 212 inakabiliwa na wimbi jipya la maambukizo ya virusi vya Corona huku hospitali zikionekana kulemewa na idadi kubwa ya wagonjwa.

Zaidi ya watu 257,000 wamekufa kwa ugonjwa wa Covid-19 nchini humo na kuifanya nchi hiyo kuwa miongoni mwa nchi zilizoathirika zaidi na janga la virusi vya Corona baada ya Marekani.

Viongozi wa majimbo walisema jana Jumanne kuwa wataungana ili kununua chanjo dhidi ya ugonjwa wa Covid-19 baada ya serikali kuu kuonekena kujikokota katika mpango wake wa utoaji chanjo.

Miji kadhaa tayari imeanza kuweka vikwazo vipya ili kuzuia kusambaa kwa virusi vya Corona.

Credit : Dw Swahili


EmoticonEmoticon