Wanafunzi 279 Waliotekwa Nyara Nigeria Waachiwa Huru

 

Mamia ya wanafunzi wa kike waliokuwa wametekwa nyara Nigeria na makundi ya wahalifu wiki iiyopita, wameachiwa huru. Gavana wa jimbo la Zamfara, Dokta Bello Muhammad Matawalle amesema wanafunzi wote 279 wameachiwa huru. 

Akizungumza na waandishi habari, Matawalle amesema kuwa jana maafisa wa serikali walifanya mazungumzo na watekaji nyara na kwamba hawakuwa na nia ya kupeleka vikosi vya usalama kwa hofu ya kuyaweka hatarini maisha ya wasichana hao. 

Awali serikali ya Nigeria ilisema wasichana waliotekwa nyara Ijumaa iliyopita kutoka kwenye mabweni yao ni 317, katika shule ya wasichana inayomilikiwa na serikali kwenye kijiji cha Jangebe.

Wasichana wana afya nzuri

Matalle amesema baada ya wasichana hao kuokolewa, walipelekwa kwenye ukumbi wa ofisi ya serikali ya jimbo la Zamfara na wote wana afya njema na wanamshukuru Mungu kwa hilo.

''Leo tumefanikiwa kuwaokoa, wasichana hawa wako nasi. Hatukulipa pesa zozote kwa ajili ya wasichana hao kuachiwa huru, kwa sababu watekaji wenyewe pia wanataka amani. 

Tutaongeza usalama kwenye eneo hili ili tukio jengine kama hilo lisitokee tena. Inshallah,'' alisema Matawalle.

Hata hivyo, wasichana wengi wanaonekana hawajapata madhara, lakini baadhi yao wamepelekwa hospitali kwa ajili ya kupatiwa matibabu. Wasichana hao walikuwa peku na wengine kati yao walikuwa na majeraha miguuni.


EmoticonEmoticon