Marekani Yaidhinisha Chanjo Ya BioNTech/Pfizer Kwa Watoto Wa 12-15

 

Mamlaka ya chakula na dawa nchini Marekani FDA imeidhinisha matumizi ya dharura ya chanjo dhidi ya virusi vya corona ya BioNTech-Pfizer kwa watoto kuanzia miaka 12 na kuendelea. 

Dr. William Gruber, mtaalamu wa chanjo ya BioNTech/Pfizer na magonjwa ya watoto iliyoko Cincinatti nchini Marekani amesema "Leo tuna furaha kubwa kusikia kwamba FDA imepanua matumizi ya dharura ya chanjo ya BNT162 B2 kwa watoto wa miaka 12 hadi 15. Kwa hiyo huu ni wakati wa nafuu kubwa kwetu, kwa kuzingatia uwezo wetu wa kupambana na janga la COVID-19."

Chanjo ya BioNTech-Pfizer ni chanjo ya kwanza kuruhusiwa kutumika kwa watoto wa chini ya miaka 16 nchini Marekani.

Taarifa ya FDA imesema takriban visa milioni 1.5 vya maambukizi kwa watoto wa kati ya miaka 11 na 17 vimeripotiwa kwenye taasisi ya kudhibiti magonjwa ya kuambukiza, CDC nchini humo tangu Aprili mwaka jana hadi Aprili 30 mwaka huu.

Mkurugenzi wa idara ya tathmini ya kibaiolojia na utafiti wa FDA Peter Marks ametoa hakikisho kuhusiana na ufanisi wa chanjo hiyo, akisema imethibitishwa kukidhi viwango vya kutumika kama dharura kwa watoto wa umri huo.

BioNTech-Pfizer na Moderna kwa pamoja zimeanza majaribio ya ufanisi wa chanjo kwa watoto wa hadi miezi sita hadi miaka 11.


EmoticonEmoticon