Ufaransa Yamaliza Shughuli Za Kijeshi Katika Eneo La Sahel

 

Rais Emmanuel Macron wa Ufaransa ametangaza kwamba operesheni za kijeshi za taifa hilo katika mapambano dhidi ya wanamgambo walio na itikadi kali katika ukanda wa Sahel zinafikia mwisho

Katika mkutano na waandishi wa habari mjini Paris kabla ya mkutano wa kilele wa mataifa saba yaliyoendelea kiviwanda ya G7, Macron amesema operesheni Barkhane itamalizika rasmi na itabadilishwa na ujumbe mwingine unaolenga kupambana na wanamgambo wa itikadi kali na utategemea zaidi washirika wa kikanda.

Kulingana na Macron, Ufaransa sasa itajielekeza zaidi katika kusambaza vikosi vyake katika ushirikiano wa pamoja na nchi za Umoja wa Ulaya, kama sehemu ya kikosi kazi kinachoitwa Takuba kinacholenga kuzidisha juhudi katika mapambano dhidi ya wanamgambo wa itikadi kali.

Aidha rais huyo amezungumzia juu ya "mabadiliko ya kina" ya operesheni za kijeshi nchini Mali na katika nchi jirani, bila ya kutoa muda kamili lakini maelezo ya kina yanatarajiwa kutolewa mwishoni mwa mwezi huu ikiwemo idadi ya wanajeshi wa Ufaransa watakaosalia.

"Mabadiliko haya yatatokea kupitia mfumo tofauti, ambao utamaanisha mfumo mpya. Hiyo ni kusema kumalizika kwa operesheni Barkhane kama operesheni ya nje, kutaruhusu ujumbe wa msaada na ushirikiano na majeshi ya kikanda na kuanzisha operesheni ya kijeshi ya kimataifa, ikijumuisha washirika wetu wote, na tukizingatia tu vita dhidi ya ugaidi."


EmoticonEmoticon