Maelfu Waandamana Ulaya Kupinga Vizuizi Vya Covid-19

 

Maelfu ya raia kwenye mataifa kadhaa ya Ulaya waliandamana siku ya Jumamosi kupinga vizuizi vya kudhibiti kusambaa ugonjwa wa Covid-19 na sera za kuwalazimisha kudungwa chanjo. 

Raia hao kwenye mataifa ya Ufaransa, Italia na Ugiriki walimiminika mitaani hususani katika miji mikuu ya nchi hizo kupaza sauti ya kupinga kulazimishwa kuchoma chanjo za Covid-19 pamoja na cheti cha kidijitali kwa wale waliopatiwa chanjo.

Wengi walioandamana wanadai sera hizo zinatishia uhuru wa raia katika wakati serikali barani Ulaya zinazidisha shinikizo dhidi ya watu amabo hawajapatiwa chanjo.

Nchini Ufaransa, kiasi watu 160,000 walijitokeza kuonesha ghadabu zao dhidi ya rais Emmanuel Macron na serikali yake mjini Paris na katika miji mingine.