Nusu Ya Raia Wa Ulaya Wamepatiwa Chanjo Kamili Ya Covid-19

 

Umoja wa Ulaya umesema zaidi ya nusu ya raia wake watu wazima wamepatiwa chanjo kamili ya Covid-19, wakati nchi barani humo na Asia zikiendelea kukabiliana na maambukizi mapya yanayochangiwa na kirusi cha Delta. 

Umoja wa Ulaya umesema watu milioni 200 wamepatiwa chanjo kamili, ikiwa ni nusu ya idadi ya watu wazima, lakini bado wameshindwa kufikia lengo la asilimia 70 hadi majira ya joto.

Kansela Angela Merkel amesema visa vya maambukizi nchini Ujerumani vinapanda kwa kiasi kikubwa. 

Ujerumani inaungana na nchi nyingine za ulaya, ambazo zimeshuhudia ongezeko la maambukizi ya Covid-19 katika wiki za hivi karibuni yanayochangiwa na kirusi cha Delta kilichogunduliwa mara ya kwanza nchini India.

Benki kuu ya Ulaya imesema wasiwasi juu ya wimbi la maambukizi inamaanisha kuwa milango ya fedha ya uokozi iko wazi ili kuhakikisha kuwa uchumi ambao ulikuwa umeanza kuimarika hauporomoki tena. 

Mkuu wa benki hiyo Christine Lagarde ameonya kuongezeka kwa wasiwasi wa kiuchumi unaotokana na kirusi cha Delta wakati benki hiyo ikiuweka vizuri mfuko wake wa uokoaji uchumi kufuatia mkutano wa baraza la wanachama wake 25.