Raisi Wa Marekani Aiwekea Vikwazo Cuba Na Kutishia Kwenda Mbali Zaidi

 

Rais wa Marekani Joe Biden ametangaza kuchukuwa vikwazo dhidi ya polisi ya Cuba Ijumaa wiki hii, akishinikizwa na mgogoro wa kisiasa unaoendelea, huku akiahidi kuwa hatua zingine zitafuata ikiwa hakutakuwa na mabadiliko "makubwa" nchini Cuba.

Alipoulizwa juu ya vikwazo vipya, rais wa Marekani amejibu, kando ya mkutano katika Ikulu ya White House na wawakilishi wa Wamarekani wenye asili ya Cuba: "Kutakuwa vikwazo zaidi, ikiwa hakutakuwa na mabadiliko makubwa nchini Cuba, jambo ambalo sitarajii" .

Siku ya Ijumaa Marekani iliidhinisha vikwazo dhidi ya maafisa wakuu wawili wa polisi wa Cuba, ikiwa ni pamoja na Polisi nzima ya Mapinduzi kwa kuhusika kwake katika ukandamizaji wa maandamano ya hivi karibuni dhidi ya serikali ya Cuba, Wizara ya Fedha ilisema.

Mkurugenzi wa PNR Oscar Callejas Valcarce na naibu mkurugenzi Eddy Sierra Arias, ambao wanatuhumiwa kwa "ukiukaji mkubwa wa haki za binadamu", wameongezwa kwenye orodha nyeusi ya Marekani.

Mali zao zimezuiliwa nchini Marekani na utumiaji wao katika mfumo wa kifedha wa Marekani sasa umezuiliwa.

"Wizara ya Fedha itaendelea kuwachukulia vikwazo na kuwatambua kwa majina wale ambao wanawezesha ukiukaji mkubwa wa haki za binadamu katika utawala wa Cuba," alibainisha mkurugenzi wa kitengo kikuu cha vikwazo katika Wizara ya Fedha, Andrea Gacki.

"Hatua zilizochukuliwa leo zinalenga kuwawajibisha wale wanaohusika na ukandamizaji wa maandamano ya amani ya raia wa Cuba na heshima kwa haki za binadamu," aliongeza.

Katika ukurasa wake wa Twitter, Waziri wa Mambo ya Nje wa Cuba Bruno Rodriguez, ameandika kwamba vikwazo vya Marekani kwa Cuba ni kinyume cha sheria na vinachukuliwa tu kiholela, akimaanisha vikwazo vya Marekani dhidi ya Cuba viliwekwa tangu mwaka 1962.