Rais Erdogan Wa Uturuki Aamuru Mabalozi 10 Wa Kigeni Kufukuzwa

 

Rais Recep Tayyip Erdogan wa Uturuki ameamuru kufukuzwa kwa mabalozi wa nchi 10, zikiwemo Ujerumani na Marekani, walioomba kuachiliwa kwa kiongozi mmoja wa asasi za kijamii mzaliwa wa Paris, Osman Kavala. 

Mabalozi hao walitowa tamko la pamoja lisilo la kawaida siku ya Jumatatu wakisema kuendelea kushikiliwa mahabusu kwa mwanaharakati na mfadhili Kavala kunaijengea mashaka Uturuki.

"Nimemuamuru waziri wetu wa mambo ya kigeni kuwatangaza mabalozi hawa 10 kwamba ni watu wasiohitajika haraka iwezekanavyo," alisema Erdogan, akitumia istihali ya kidiplomasia inayomaanisha hatua ya kwanza kabla ya ufukuzwaji.

"Lazima waondoke hapa siku ile ile wasiyoijuwa tena Uturuki," aliongeza, akiwatuhumu mabalozi hao kwa "utovu wa adabu."

Siku ya Jumamosi (Oktoba 23), Erdogan alimuelezea Kavala kama "wakala" wa bilionea wa Kimarekani aliyezaliwa Hungary, George Soros, ambaye amekuwa akiandamwa mara kwa mara na wanasiasa wa mrengo wa kulia na wenye nadharia za hujuma dhidi ya Mayahudi.