Bunge La Ujerumani Laidhinisha Sheria Mpya Za Kudhibiti Corona

 

Bunge la Ujerumani limeidhinisha sheria mpya kukabiliana na ongezeko la maambukizi ya virusi vya Corona, wakati Kansela Angela Merkel anayekaimu serikali akijiandaa kukutana na viongozi wakuu wa majimbo 16 ya Ujerumani. 

Bunge la Ujerumani limeidhinisha sheria mpya za kukabiliana na ongezeko la maambukizi ya virusi vya Corona. 

Hatua hiyo imechukuliwa wakati Kansela Angela Merkel anayekaimu serikali, akijiandaa kukutana na viongozi wakuu wa majimbo 16 ya Ujerumani kujadili hatua zaidi za kukabiliana na janga la virusi hivyo. 

Janga la virusi vya Corona linatishia kuvuka viwango nchini Ujerumani-katika mkoa wa Bayern, Kusini mwa Ujerumani katika eneo la Freising, inaelezwa kwamba vitanda vya wagonjwa katika wodi za wagonjwa mahututi vimejaa na wafanyakazi wa huduma ya afya nao pia wamepungua.

Hospitali ya eneo hilo la Freising imefikia uamuzi ambao haukutarajiwa wa kumhamishia kaskazini mwa Itali mgonjwa mmoja wa Covid kwa ajili ya matibabu.

Wakati maambukizi yakitajwa kuongezeka bunge la nchi hii limepiga kura na kupitisha sheria kadhaa jana Alhamisi zilizopendekezwa na vyama ambavyo vina uwezekano wa kuunda serikali ijayo ya shirikisho.