Davido Asema Mashabiki Walimtuma £300,000 Baada Ya Kuwaomba Kupitia Twitter

 

Nyota wa Afrobeats Davido anasema mashabiki wamemtumia takriban pauni 300,000 baada ya kuwataka wamtumie pesa kwenye Twitter.

Mwimbaji huyo aliomba mashabiki wanaoamini kuwa "nimekupa wimbo unaovuma" "nitumie pesa", kabla ya kuweka jina lake halisi, David Adeleke, na nambari ya akaunti ya benki.

Picha za skrini alizotoa mtandaoni zinaonyesha kuwa amekusanya zaidi ya Naira milioni 170 za Nigeria (kama pauni 300,000).

Newsbeat imemtaka Davido kutoa maoni yake lakini bado hajajibu.

Davido - ambaye alitumbuiza katika chumba cha mapumziko cha 1Xtra mwezi Machi mwaka huu - anachukuliwa kuwa mmoja wa mastaa wakubwa wa Kiafrika duniani.

Mwanamuziki huyo alituma ujumbe kwenye ukurasa wake wa Twitter kuwa lengo lake lilikuwa ni kutaka mashabiki wamtumie Naira milioni 100 ili kuondoa gari lake la Rolls Royce kutoka bandari ya Nigeria, ili aweze kulipa bili ambazo hazijalipwa ili kuachilia bidhaa iliyosafirishwa kutoka nje ya nchi.

Abubakr mwenye umri wa miaka 23 ni shabiki mkubwa wa Davido na anasema kumtumia pesa "ni jambo lililokamilisha siku yake".

"Nilifanya hivyo kwa upendo. Najua yeye ni tajiri zaidi yangu na watu wanasema kwa nini nifanye hivyo," anaiambia Radio 1 Newsbeat.

"Inanifanya nijisikie mwenye furaha. Inahisi kama moja ya malengo yangu yamefikiwa. Ni nadra kwa shabiki kufanya miamala na mtu mashuhuri."

Wakati baadhi ya mashabiki wake wamefurahi zaidi kutuma pesa wengine wamemkosoa mwimbaji huyo.

Mtumiaji mmoja aliandika katika twitter: "Ulimwengu unaenda wazimu, Davido anawezaje kuwauliza mashabiki [pesa]?"

Lakini wengine hawakukubali, huku mmoja akisema: "Anastahili zaidi... amekuwa baraka kwa wengi na ni wakati wa kumrudishia. Happy birthday in advance @davido."

Wengi wameshiriki picha za skrini za uhamisho wa benki kwa nyota huyo wa Nigeria kujibu chapisho lake la kwanza.

Davido mara nyingi hushiriki picha kwenye Instagram akiwa kwenye jeti binafsi, au akiwa na magari ya kifahari na vito vya bei ghali.