Jeshi La Sudan Lamrejesha Madarakani Waziri Mkuu Abdalla Hamdok

 

Waziri Mkuu wa Sudan aliyeondolewa Abdalla Hamdok amerejeshwa madarakan, baada ya kuwekwa katika kifungo cha nyumbani wakati wa mapinduzi ya ghafla ya kijeshi mwezi uliopita.

Bw. Hamdok aliachiliwa kutoka kifungo cha nyumbani mapema leo kabla ya kuonekana kwenye Televisheni ya serikali pamoja na kiongozi wa mapinduzi, Jenerali Abdel Fattah al Burhan, katika hafla ya kutia saini makubaliano.

Waziri Mkuu alisema amekubali kusaini mkataba wa kisiasa ili kulinda maisha ya raia.

Makabiliano kati ya waandamanaji wanaounga mkono demokrasia na vikosi vya usalama yamekuwa ya umwagaji damu katika siku za hivi karibuni. Makumi ya watu wamepigwa risasi na kuuawa tangu jeshi lilipochukua mamlaka tarehe 25 Oktoba.

Hapo awali, wapatanishi walitangaza kuwa makubaliano yaliyofikiwa ni pamoja na kuachiliwa kwa wafungwa wa kisiasa.

Majenerali wa kijeshi wa Sudan wamekuwa chini ya shinikizo la kuwataka kuirejesha kazini serikali inayoongozwa na raia iliyoiondoa madarakani mwezi uliopita

Hatua iyo Ilizua maandamano makubwa ya wiki kadhaa ambayo yalisababisha vifo vya watu wengi.

Makubaliano hayo yaliafikiwa Jumamosi usiku, na yatatiwa saini kutekelezwa baadaye Jumapili, mkuu wa Chama cha Umma cha Sudan, Fadlallah Burma Nasir, alithibitisha.