Mwanamke Akata Sehemu Za Siri Za Mumewe Kufuatia Mzozo Wa Kinyumbani

 

Mzee mmoja mwenye umri wa miaka 60 kutoka kijiji cha Kirindara, eneo bunge la Igembe ya kati Kaunti ya Meru nchini Kenya anauguza majeraha katika hospitali ya Nyambene Level 4 baada ya mkewe kukata sehemu zake za siri usiku wa Ijumaa.

Mwanamume huyo ambaye ni mwalimu mstaafu alikatwa sehemu zake za siri na mkewe Esther Meeme aliyekuwa amejawa na ghadhabu kufuatia mzozo wa kinyumbani.

Mwanamume huyo alikumbana na masaibu hayo katika kitanda chao cha ndoa ambapo mkewe alimfunga kamba na kuanza kiungo chake cha uzazi.

Kando na kupoteza uume wake, mwanaume huyo pia alipata majeraha mengine kichwani kutokana na kichapo.

Kwa bahati aliokolewa na wanafamilia wake na kukimbizwa katika hospitali ya Nyambene level 4 ambako anapigania maisha yake.

 Akithibitisha kisa hicho chifu wa eneo hilo Murungi Matundu alisema mhalifu tayari yuko kizuizini katika kituo cha polisi cha Kangeta akisubiri kufikishwa kortini.

Matundu alilaani vikali kitendo hicho na kukitaja kuwa ni cha unyama na kinyume cha sheria huku akisema suala hilo ameliachia polisi kwa uchunguzi zaidi.

"Chochote alichokifanya mwanamke huyu ni kibaya na hakijasikika katika jamii ya Wameru," chifu alilalamika na kuongeza kuwa, "maswala ya nyumbani yanapaswa kushughulikiwa kwa busara na sio mihemko ili familia isitawi kwa amani."

Aidha amewatahadharisha wananchi kutojichukulia sheria mkononi bali watoe taarifa kwa mamlaka husika.