BOMU LALIPUKA NA KULETA MAAFA KARIBU NA UWANJA WA NDEGE SOMALIA

Takriban watu wanane wameuawa katika mlipuko wa bomu katika mji mkuu wa Somalia, Mogadishu, waokoaji wamesema.

Kundi la wapiganaji wa Kiislamu la al-Shabab limesema lilitekeleza shambulio hilo.

Mlipuko huo ulitokea kwenye barabara ya eneo la kuingia kambi ya Jeshi la wana anga la Somalia ambalo iko karibu na uwanja wa ndege wa kimataifa.

Walioshuhudia tukio hilo wameliambia shirika la habari la AFP kwamba msafara wa usalama wa kibinafsi, ukiwasindikiza wageni, ulikuwa ukipita wakati bomu hilo likilipuka.

"Mlipuko huo ulikuwa mkubwa kiasi kwamba umeharibu majengo mengi yaliyo karibu na barabara na magari yanayopita eneo hilo," Hassan Nur alisema.

Kundi la wanamgambo wa Kiislamu la Al Shabab mara kwa mara hutekeleza mashambulizi ya kujitoa mhanga.

Somalia pia iko katikati ya mzozo wa kisiasa kutokana na mzozo wa madaraka kati ya rais na waziri mkuu kabla ya uchaguzi.