RAIA WA RWANDA WAKIMBIA NCHI YAO KWA KUOGOPA KUPATA CHANJO YA COVID-19


Raia wa Rwanda wapatao 100 wamevuka mpaka na kuingia nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, katika siku za hivi karibuni, kwa kile wanachokisema wanakimbia nchi yao kwa sababu ya masharti ya kupata chanjo, ili kupambana na janga la Covid-19.

Ripoti zinasema raia hao wa Rwanda, walivuka mpaka na kuingia DRC kusini mwa kisiwa cha Ijwi, kilichoko kwenye Ziwa Kivu, mpakani mwa Rwanda na DRC, wakitumia mitumbwi,

Mmoja wa maafisa wa serikali za mitaa upande wa Rwanda ambaye hakutaka jina lake kutajwa, amezungumzia suala hili.

Lakini upande wa DRC kuwasili kwa wakimbizi hawa kumezua hali ya sintofahamu ambapo msimamizi wa eneo la Ijwi, Karongo Kalaja, amesema bado hazijulikani sababu za kweli kwa nini raia hao wa Rwanda wanaikimbia nchi yao.

Professa Daddy Swaleh Samuel ambaye ni mwenyekiti wa shirika lisilokuwa la kiserikali linalotetea masilahi ya vijana katika kukuza Utamaduni la AJPC ameshuhudia kuingia kwa raia hao wa Rwanda katika ardhi ya DRC.

Nchini Rwanda, chanjo dhidi ya Covid-19 ni ya lazima katika usafiri wa umma, kwenye baa na mikahawa au hata wakati wa mikutano.