RAIA WALIOKIMBIA NCHI KWAAJILI YA CHANJO WARUDISHWA MAKWAO

Raia wa Rwanda zaidi ya 100 waliokuwa wamevuka mpaka na kuingia nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo kwa kile walichokisema walikimbia kulazimishwa kupata chanjo dhidi ya virusi vya Covid 19, wamerejeshwa nyumbani.

Serikali ya DRC inasema raia hao wa Rwanda waliokuwa wanaishi katika kisiwa cha Ijwi, ziwani Kivu, wamerejeshwa katika nchi yao Alhamisi asubuhi.

Imebainika kuwa raia hao wa Rwanda wapatao 101, walikuwa ni pamoja na wanaume, wanawawake na watoto waliowasili katika kisiwa hicho kwa usafiri wa boti.

Msemaji wa serikali ya Rwanda Yolande Makolo siku ya Jumatano alisema watu hao walikuwa wametoroka ili kukwepa chanjo kwa sababu za kiimani, lakini wataelimishwa kuhusu manufaa ya chanjo.