SHIRIKA LA AFYA LAONYA NUSU YA BARA LA ULAYA ITAAMBUKIZWA OMICRON

Shirika la Afya Ulimwenguni limeonya kwamba nusu ya bara Uropa itakuwa imeambukizwa kirusi cha Covid -Omicron ndani ya wiki sita hadi nane zijazo.

Dk Hans Kluge alisema "wimbi la kutokea magharibi hadi mashariki" la Omicron lilikuwa likienea katika eneo lote, juu ya kuongezeka kwa aina ya kirusi cha Delta.

Makadirio hayo yalitokana na kesi mpya milioni saba zilizoripotiwa kote Uropa katika wiki ya kwanza ya 2022.

Idadi ya maambukizo imeongezeka zaidi ya mara mbili katika kipindi cha wiki mbili.

"Leo kirusi cha Omicron iknawakilisha wimbi jipya la mawimbi kutoka magharibi hadi mashariki, linaloenea katika eneo lote juu ya kuongezeka kwa Delta ambayo nchi zote zilikuwa zikisimamia hadi mwishoni mwa 2021," Dk Kluge aliambia mkutano wa wanahabari.

Alinukuu Taasisi ya takwimu na Tathmini ya Afya yenye makao yake makuu mjini Seattle ikitabiri kwamba "zaidi ya asilimia 50 ya wakazi katika eneo hilo wataambukizwa na Omicron katika muda wa wiki sita hadi nane zijazo".

Alisema nchi za Ulaya na Asia ya Kati zimesalia chini ya "shinikizo kubwa" wakati virusi vikienea kutoka nchi za magharibi hadi Balkan.

"Jinsi kila nchi inavyojibu lazima ifahamishwe na hali yake ya magonjwa, rasilimali zilizopo, hali ya kuchukua chanjo na muktadha wa kijamii na kiuchumi", aliongeza.

Uchunguzi wa hivi majuzi unaonyesha kuwa Omicron ina uwezekano mdogo wa kuwafanya watu kuwa wagonjwa sana kuliko aina nyingine za awali za Covid. Lakini Omicron bado inaambukiza sana na inaweza kuwaambukiza watu hata kama wamechanjwa kikamilifu.

Idadi ya rekodi ya watu wanaoipata imeacha mifumo ya afya chini ya mkazo mkubwa.