TAKRIBANI WATU 20 WAFA MOTO NEW YORK

Watu 19 wakiwemo watoto 9 wamekufa Jumapili kutokana na moto kwenye kitongoji ya Bronx mjini New York, ukiwa mkasa uliolezewa kuwa mbaya zaidi na mkuu wa zima moto mjini humo katika miaka ya karibuni.

Mshauri mkuu wa meya wa New York Eric Adams Jumapili amedhibitisha vifo hivyo wakati afisa mmoja wa jiji ambaye hakuruhusiwa kuzungumza hadharani akidhibitisha vifo vya watoto.

Darzeni ya watu pia wanasemekana kujeruhiwa wakati wa moto huo,13 miongoni mwao wakisemekana kuwa katika hali mahututi. Idara ya moto ya New York imesema kwamba zaidi ya wazima moto 200 walishiriki kuzima moto huo kwenye nyumba za makazi za Twin Park.

Mkuu wa idara ya zima moto ya New York Daniel Nigro wakati akizungumza na wanahabari amesema kwamba wazima moto walipata watu waliokufa katika kila orofa la jengo hilo lenye orofa 19, wengi wakisemekana kuangamizwa na moshi mkali.

Nigro amelinganisha mkasa huo na ule wa 1990 kwenye klabu cha Happy Land ambao uliuwa watu 87 baada ya mmoja wa wateja kuuwasha kutokana na kufukuzwa kutoka kwenye klabu hicho, kufuatia majibizano na mpenzi wake.