UINGEREZA YASHAURIWA KUTOANZA KUTOA CHANJO YA NNE ZAIDI YA CORONA

 

Kamati ya ushauri kwa serikali ya Uingereza imepinga utoaji wa chanjo ya nne dhidi ya COVID-19 kwa watoa huduma majumbani na wazee wenye zaidi ya miaka 80 kwa kuwa takwimu zinaonyesha kwamba dozi ya tatu inatoa ulinzi wa muda mrefu na kuwaepusha kulazwa hospitalini. 

Mwenyekiti wa kamati ya washauri hao Profesa Wei Shen Lim amesema takwimu zinaonyesha dozi ya tatu ya chanjo imeendelea kutoa ulinzi wa kiwango cha juu dhidi ya maambukizi hayo kuwa mabaya zaidi, hata kwa kundi la wazee ambalo huwa hatarini zaidi. 

Na kwa maana hiyo kamati hiyo inasema hakuna umuhimu wa kuanzisha chanjo nyingine ya ziada ingawa wamesema wataendelea kutathmini hatua hiyo. 

Takriban asilimia 90 ya watu walio zaidi ya miaka 65 hawakulazwa hospitalini miezi mitatu tangu walipopata chanjo ya ziada ya tatu hii ikiwa ni kulingana na takwimu zilizokusanywa na shirika la usalama wa afya nchini humo, HSA.