ZAIDI YA WATU 164 WAMEUAWA NA WENGINE WENGI KUJERUHIWA KAZAKHSTAN

Takriban watu 164 wamekufa nchini Kazakhstan wakati wa maandamano ya kupinga serikali, kwa mujibu wa ripoti za vyombo vya habari zilizowanukuu maafisa wa afya.

Iwapo itathibitishwa itaashiria ongezeko kubwa kutoka kwa idadi ya awali ya vifo 44.

Takriban watu 6,000 wamekamatwa, ikiwa ni pamoja na "idadi kubwa ya raia wa kigeni", ofisi ya rais ya Kazakhstan ilisema Jumapili.

Maandamano hayo, yaliyochochewa na kupanda kwa bei ya mafuta, yaligeuka kuwa ghasia kubwa huku yakienea nchini kote.

Walianza tarehe 2 Januari na walikua wakionesha kutoridhika na serikali na Rais wa zamani Nursultan Nazarbayev, ambaye aliongoza Kazakhstan kwa miongo mitatu, bado anafikiriwa kuwa na ushawishi mkubwa.

Wiki iliyopita, wanajeshi kutoka nchi zikiwemo Urusi walitumwa Kazakhstan kusaidia kurejesha utulivu.

Taarifa ya rais imeongeza kuwa hali imetulia, huku wanajeshi wakiendelea na operesheni za "usafishaji" na kulinda "vifaa vya kimkakati".

Hali ya hatari na amri ya kutotoka nje kwa nchi nzima imesalia.